JAJI MKUU WA ZANZIBAR AFUNGUA MAFUNZO YA e-CMS
2026-01-30
Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwa kuanzishwa kwa Mfumo wa Uendeshaji wa Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (e-CMS) ni sehemu ya mageuzi ya kimkakati ya Mahkama, yanayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mashauri.\r\nAkizungumza wakati akifungua mafunzo ya majaribio ya utumiaji wa mfumo huo yanayofanyika Hotel Verde Mjini Magharibi Unguja, amesema Mfumo wa Uendeshaji wa Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (e-CMS), ni hatua muhimu katika kuboresha utoaji wa haki kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hivyo kuifanya Mahkama kuondokana na mfumo wa makaratasi, ambao una changamoto nyingi ikiwemo ucheleweshaji wa mashauri, upatikanaji hafifu wa taarifa za kesi, pamoja na ugumu wa kupata nakala za mwenendo na hukumu kwa wakati.\r\nAmebainisha kuwa, Mahkama imekamilisha ujenzi wa moduli zote muhimu za mfumo huo, zikiwemo uthibitishaji na uidhinishaji wa watumiaji, usajili na upangaji wa mashauri, uundaji wa mafaili ya kidijitali, mchakato wa usikilizwaji wa kesi, utoaji wa maamuzi pamoja na malipo kwa njia ya kielektroniki. Majaribio ya sasa yanakusudia kutoa fursa kwa wadau na watumiaji kupima vipengele hivyo na kutoa maoni ya maboresho kabla ya kuanza matumizi rasmi.\r\nAkielezea faida za mfumo wa e-CMS, Jaji Mkuu amesema mfumo huo utawezesha kumalizika kwa mashauri kwa haraka na kupunguza mrundikano wa kesi Mahkamani, kurahisisha wananchi kufungua na kufuatilia mashauri yao wakiwa popote duniani, pamoja na kupata taarifa za kesi, mwenendo na maamuzi kwa wakati kupitia vifaa vya kidijitali ikiwemo simu za mkononi.\r\nJaji Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa Mahkama na wadau wote kujiandaa kikamilifu kuutumia mfumo wa e-CMS, ikiwa ni pamoja na kubadilika kutoka mifumo ya kazi ya awali na kuendana na mazingira ya kidijitali. Amesisitiza kuwa mfumo huo unaunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha huduma za kijamii na utoaji wa haki kwa wananchi.\r\nNae mratibu wa Mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP) Mhe. Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim amesema kuwa utekelezaji wa Mfumo wa Uendeshaji wa Mashauri kwa Njia ya Kielektroniki ni sehemu ya Mradi wa Maboresho ya Mahkama unaojengwa juu ya vipengele vikuu vitatu ambavyo ni kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi (Access to Justice), kuboresha ufanisi katika utoaji wa huduma za Mahkama (Efficiency), pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa wadau wote wa haki kwa ujumla.\r\nJaji Ibrahim ameongeza kuwa mfumo huo umetengenezwa na wataalamu wa TEHAMA kutoka Mahkama ya Zanzibar kwa kushirikiana na wataalamu wenzao kutoka Mahkama ya Tanzania Bara, sambamba na mchango wa wataalamu wengine kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ushirikiano huo umeiwezesha Mahkama kupata mfumo unaokidhi viwango vya kitaalamu na mahitaji halisi ya mazingira ya utoaji haki nchini.\r\nAmesema, Mahkama pia imepanga kuchukua hatua nyingine muhimu kabla ya kuanza matumizi rasmi ya mfumo huo, ikiwemo ukaguzi wa utayari wa mfumo na miundombinu, kuanzishwa kwa timu ya msaada wa kiufundi, pamoja na ufuatiliaji wa utendaji wa mfumo na ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya maboresho endelevu.\r\nAidha, ameishukuru Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP) kwa kuwezesha utekelezaji wa mfumo huo na mradi kwa ujumla wake.