Skip to main content

New e-CMS system launching February 1, 2026 | Learn more

DC MJAJA ASHAJIHISHA MATUMIZI YA TEHAMA KWA WANANCHI

2026-02-07 Zanzibar Judiciary
MHE. MJAJA ASHAJIHISHA MATUMIZI YA TEHAMA KWA WANANCHI\r\nMkuu wa Wilaya ya Micheweni Mhe. Khatibu Juma Mjaja, amesema kuwa uimarishaji wa mifumo ya kielektroniki katika Mahkama utapunguza kwa kiasi kikubwa kilio cha wananchi kinachotokana na ucheleweshwaji wa usajili, usikilizaji na uendeshaji wa mashauri.\r\nAkizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Wiki ya Sheria lililofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete-Pemba, Mhe. Mjaja ameeleza kuwa matumizi ya TEHAMA si tu yanarahisisha usajili na usikilizaji wa mashauri, bali pia yana mchango mkubwa katika kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi, kwa kuokoa muda wa kwenda Mahkamani na gharama zake.\r\nAidha, amewaasa washiriki wa kongamano hilo kutumia fursa hiyo muhimu kupata elimu ya kisheria itakayosaidia kuibadilisha jamii kifikra na kimatendo, hatua itakayochangia kuleta maendeleo na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.\r\nMhe. Mjaja amebainisha kuwa Mahkama zimepiga hatua kubwa kwa kuachana na mifumo ya kizamani na kuanza kutumia mifumo ya kisasa inayokwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia, hatua inayolenga kurahisisha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi kwa ufanisi na kwa wakati.\r\nMwisho, Mgeni Rasmi aliishukuru Mahkama kwa kumualika kuwa sehemu ya kongamano hilo muhimu, akieleza kuwa anaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Mahkama katika kuimarisha utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwa wananchi.\r\nNae Naibu Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Hussein Makame Hussein, amesema kuwa Mahkama imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha na kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka, kwa usawa na kwa gharama nafuu.\r\nMhe. Hussein alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Mahkama, kupunguza msongamano wa mashauri na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahkama, akisisitiza kuwa elimu ya matumizi ya mifumo hiyo kwa wadau wa haki ni jambo la msingi katika kufanikisha dhamira hiyo.\r\nAidha, ameeleza kuwa Kongamano hilo limefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Matumizi ya TEHAMA ni Chachu ya Upatikanaji wa Haki”, kauli mbiu inayodhihirisha dhamira ya Mahkama katika kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia kwa lengo la kuboresha huduma za haki nchini.