Skip to main content

New e-CMS system launching February 1, 2026 | Learn more

JAJI MKUU WA ZANZIBAR AFUNGUA MAFUNZO YA MFUMO WA eCMS KWA MAJAJI WA MAHKAMA KUU ZANZIBAR, MAKADHI, WARAJIS NA WAKUU WA TAASISI

2026-03-27 Zanzibar Judiciary
JAJI MKUU WA ZANZIBAR AFUNGUA MAFUNZO YA MFUMO WA eCMS KWA MAJAJI WA MAHKAMA KUU ZANZIBAR, MAKADHI, WARAJIS NA WAKUU WA TAASISI \r\nJaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwa Mahkama ya Zanzibar inategemea kuanza rasmi matumizi ya mfumo wa Uendeshaji wa Mashauri Kielektroniki (e-CMS) mara tu baada ya kupatiwa mafunzo ya mfumo huo watendaji na wadau wote wa Mahkama, ikiwa ni hatua muhimu ya kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa haki kwa wananchi. \r\nJaji mkuu ameeleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, Warajis, Makadhi na Wakuu wa Taasisi za DPP, AG, Polisi, ZAECA, Mafunzo, yanayofanyika katika Hoteli ya Kwanza iliyopo Kizimkazi Wilaya ya Kusini Unguja.\r\nAidha Mhe Jaji Mkuu amesema matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki siyo tena chaguo, bali ni hitaji la lazima katika dunia ya sasa. Mfumo wa usikilizaji wa Mashauri kwa njia ya kieletronik utasaidia kwa kiasi kikubwa kuharakisha usikilizaji wa kesi, kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri, na kuongeza uwazi pamoja na ufanisi katika Mahkama .\r\nAidha, ameeleza kuwa mfumo huo utawezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa mrundikano wa mashauri mahkamani kwa kurahisisha uendeshaji wake na wananchi wataweza kufungua na kufuatilia kesi zao wakiwa popote bila kufika mahakamani, pamoja na kupata taarifa muhimu kupitia simu zao, ambapo, mfumo utaunganishwa na tovuti ya Mahkama na programu za simu ili kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma zake.\r\nJaji Mkuu amewataka wadau wote kushiriki kikamilifu na kwa umakini katika mafunzo ya matumizi ya mfumo huo, akisisitiza kuwa si hiari bali ni wajibu wa kitaifa. Aidha, amefafanua kuwa majaribio ya mfumo yataanza rasmi mnamo Aprili 2 hadi Mei 2, 2026 kabla ya uzinduzi rasmi, huku akieleza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria katika kuimarisha utoaji wa haki Zanzibar.\r\nAkizungumza katika mafunzo hayo, mratibu wa Mradi wa Maboresho ya Mahkama Zi-JUMP, Mhe. Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kwa wadau wa ndani wa Mahkama ili kuwawezesha kuutumia mfumo huo kwa ufanisi kabla ya kuwahusisha wadau wengine wa nje, ambapo ameeleza kuwa miongoni mwa wadau wanaoshiriki katika mafunzo ya mfumo huo ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (AG), Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA).\r\nAidha, Jaji Ibrahim alisisitiza kuwa mafanikio ya mfumo huo yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa wadau wote wa sekta ya sheria, akibainisha kuwa bila ushirikiano huo, mfumo huo hautaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa, hususan katika kuimarisha uwazi na ufanisi wa utoaji wa haki.\r\nAmefafanua kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria katika kuibadilisha Mahakama ya Zanzibar kuwa taasisi ya kisasa inayokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia, huku ikitarajiwa kuongeza imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji \r\nUjenzi wa mfumo wa e-CMS ulianza Agosti 1, 2025 na kukamilika Februari 2026, ukihusisha wataalamu wa TEHAMA kutoka Mahakama ya Tanzania, Mahkama ya Zanzibar pamoja na taasisi nyingine za ndani, na utaanza majaribio ya matumizi Aprili 2 hadi Mei 2, 2026, kabla ya kutangaza tarehe rasmi ya kuanza matumizi kamili (Go Live), kulingana na mafanikio ya hatua ya majaribio.\r\nMafunzo hayo ni sehemu ya maboresho makubwa kupitia Mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ukiwa na lengo kurahisisha huduma za kimahkama, kuboresha utendaji kazi na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji wa haki