DKT. UKI AFUNGUA MAFUNZO YA UKAZAJI HUKUMU WA AMRI ZA MAHKAMA
2026-05-16
Zanzibar Judiciary
Mkuu wa Skuli ya Sheria Zanzibar, Dkt. Ali Uki amesema mafunzo ya Ukazaji wa Hukumu na Amri za Mahkama yatachangia kuimarisha utendaji wa Mahkama pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki nchini.\r\n\r\nDkt. Uki amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Ukazaji wa Hukumu na Amri za Mahkama kwa Mahakimu na Makadhi yaliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Uwanja wa Ndege Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.\r\n\r\nDkt. Uki amesema Mafunzo haya yamekuja katika wakati muafaka ambapo Mahkama ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa haraka, kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki za binadamu. Ni muhimu kwa Mahakimu na Makadhi kuwa na uwezo wa kuandika hukumu zinazozingatia weledi, maadili ya kazi na matumizi sahihi ya sheria.\r\n\r\nAmesema kuwa baadhi ya sheria zilizopo bado zinakwamisha utoaji wa hukumu na upatikanaji wa haki kwa wakati, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo washiriki katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kimahkama.\r\n\r\nPia amewataka washiriki kutoridhika na viwango vya elimu walivyonavyo hivi sasa, badala yake waendelee kujiongezea maarifa kupitia warsha, makongamano na kujiendeleza kielimu katika vyuo vikuu huria ili kuongeza uwezo wao wa kitaaluma.\r\n\r\nKwa upande wake, Mrajis wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mhe. Valentina A. Katema amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini katika kufuatilia mada zitakazowasilishwa na kuhakikisha wanatumia elimu na ujuzi watakaoupata katika kuboresha utendaji wao wa kazi wa kila siku.\r\n\r\nAmesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya kuimarisha uwezo wa watumishi wa Mahkama katika kutoa huduma bora, za haki na zenye kuzingatia misingi ya taaluma na maadili ya kazi. \r\n\r\nAidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na matumizi sahihi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya taasisi hiyo.\r\n\r\nMafunzo hayo ni miongoni mwa sehemu ya mradi wa Maboresho ya Mahkama ya Zanzibar (Zi-JUMP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).