Skip to main content

New e-CMS system launching February 1, 2026 | Learn more

JAJI MKUU WA ZANZIBAR AFUNGUA MAFUNZO YA KUSHUGHULIKIA MIGOGORO YA MIRATHI

2026-05-25 Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Ramdhan Khamis Abdalla, amesema kuwa mafunzo kuhusu namna ya kushughulikia migogoro ya mirathi yatawasaidia kuongeza uwezo na uelewa wa kina katika kutatua changamoto zinazohusiana na masuala ya mirathi, jambo ambalo litachangia kuimarisha utoaji wa haki kwa wananchi na kupunguza migogoro katika jamii.rnMhe. Jaji Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kushughulikia migogoro ya mirathi yaliyofanyika katika Hoteli ya Mdinat Al Bahr iliyopo Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi. Ambapo mafunzo hayo yamejumuisha Majaji wa Mahkama kuu ya Zanzibar pamoja na washiriki mbalimbali katutoka katika taasisi zenye jukumu la kushughulikia masuala ya mirathi ikiwemo Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.rnAmesema kuwa migogoro ya mirathi ni miongoni mwa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika jamii na wakati mwingine husababisha migawanyiko ndani ya familia pamoja na kuathiri mahusiano ya kijamii. Amesisitiza kuwa kutokuwepo kwa uelewa wa kutosha kuhusu sheria, taratibu na haki za wahusika mara nyingi huwa chanzo cha migogoro hiyo kuendelea kwa muda mrefu.rnAidha, Mhe. Jaji Mkuu amefahamisha kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa washiriki kutokana na mchango wake katika kuongeza maarifa na kuwajengea uwezo wa kushughulikia kesi na migogoro ya mirathi kwa ufanisi zaidi, na ni wajibu wa washiriki kuyapa uzito mafunzo yote yatakayotolewa ili waweze kupata maarifa yatakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.rnPia amewataka washiriki kutumia nafasi hiyo kujifunza, kuuliza maswali na kubadilishana uzoefu unaoweza kusaidia kuboresha utendaji kazi wao, huku akieleza kuwa elimu inayopatikana kupitia mafunzo hayo itakuwa na manufaa makubwa si kwa washiriki pekee bali pia kwa jamii nzima inayotarajia kupata huduma bora na haki stahiki.rnKwa upande mwingine ameeleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo washiriki katika mbinu mbalimbali za kushughulikia migogoro ya mirathi kwa njia ya haki, usawa na kufuata misingi ya sheria, na inatarajiwa kuwa maarifa yatakayopatikana yatachangia kupunguza migogoro ya mirathi katika jamii pamoja na kuimarisha mfumo wa utoaji wa haki Zanzibar.rnMafunzo hayo yanafanyika chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP).