Skip to main content

New e-CMS system launching July 1, 2026 | Learn more

JAJI MKUU WA ZANZIBAR ASISITIZA UTEKELEZAJI WA MABORESHO YA MAHKAMA KWA MANUFAA YA WANANCHI

2026-08-10 Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutekeleza kwa ufanisi maboresho ya Mahkama ya Zanzibar, akieleza kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia.\r\n\r\nMhe. Jaji Mkuu ameyasema hayo katika viwanja vya Mahkama Kuu iliyopo Tunguu wakati aliposhuhudia utiaji saini wa mikataba wa majengo mapya matano ya Mahkama na ukarabati majengo mawili ya Mahkama. Ujenzi huo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 49 za kitanzania.\r\n\r\nAidha alisema Miundombinu bora ya Mahkama ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki katika mazingira salama, rafiki na yenye kuheshimu utu wa kila mtu. Dhamira ya Mahkma si kujenga majengo kwa ajili ya uzuri pekee, bali kujenga mazingira yatakayochangia utoaji wa haki kwa wakati, kwa ufanisi na kwa usawa.\r\n\r\nJaji Mkuu ameeleza kuwa Mahkama ya Zanzibar imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha utoaji wa huduma za kimahkama, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika usimamizi na usikilizaji wa mashauri, uboreshaji wa miundombinu pamoja na kuongeza ufanisi wa watendaji wa Mahakama.\r\n\r\nKwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Dkt. Mwalimu Haroun Ali Suleiman amewataka wakandarasi kuhakikisha miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa maboresho ya Mahkama inakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.\r\n\r\nMhe. Haroun amewataka wakandarasi na wadau wanaohusika na utekelezaji wa miradi hiyo kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha fedha na rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maboresho ya Mahkama zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.\r\n\r\nAidha, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahkama pamoja na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha miundombinu ya Mahkama inaboreshwa na huduma zinawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi. Akisistiza kuwa maboresho hayo ni muhimu katika kujenga mfumo wa haki unaokidhi mahitaji ya wananchi na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayotokea duniani.\r\n\r\nNae mwakilishi wa Benki ya Dunia Nd. Benjamin Ndazi Mtesigwa ameeleza kwamba dhamira ya taasisi hiyo ni kuendelea kushirikiana na Mahkama ya Zanzibar katika utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Mahkama ya Zanzibar (Zi-JUMP).\r\n\r\nAmesema Benki ya Dunia inatambua umuhimu wa maboresho yanayofanyika katika Mahkama ya Zanzibar, hususan katika kuongeza upatikanaji wa haki, kuboresha ufanisi wa huduma za Mahkama na kuongeza uwazi.\r\n\r\nNd. Mtesigwa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Benki ya Dunia, Serikali na Mahakama ya Zanzibar ili kuhakikisha malengo ya Zi-JUMP yanafikiwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi. \r\nAkifafanua kuwa Maboresho hayo yanatarajiwa kuendelea kuimarisha Mahkama ya Zanzibar na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki zilizo bora, za haraka, za uwazi na zinazozingatia matumizi ya teknolojia.