Skip to main content

New e-CMS system launching July 1, 2026 | Learn more

MAHKAMA YA ZANZIBAR KUTOA ELIMU KWA MASHEHA , WASAIDIZI WA SHERIA ( PARALEGO) VIONGOZI WA DINI, MAKUNDI YA WANAWAKE NA VIJANA WA MKOA WA KUSINI PEMBA

2026-09-19 Zanzibar Judiciary
Kaimu Mrajis wa Mahkama ya Zanzibar, Mhe. Khamis Rashid Khamis, amesema Mahkama imedhamiria kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utoaji wa haki kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.\r\nMhe. Khamis ameyasema hayo tarehe 19 Septemba 2026 wakati akifungua mafunzo kuhusu Dhamira ya Mabadiliko ya Mahkama, yaliyojumuisha Masheha, Wasaidizi wa Sheria pamoja na baadhi ya Viongozi wa Dini kutoka Mkoa wa Kusini Pemba. Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Baraza la Mji Chake Chake, Pemba.\r\nAlieleza kuwa Masheha, Viongozi wa Dini, Wasaidizi wa Sheria, wanawake na vijana wana nafasi kubwa katika jamii. Kila siku wanakutana na wananchi wenye changamoto mbalimbali zinazohitaji ushauri, mwongozo au kupata taarifa sahihi kuhusu haki zao. Hivyo , Mahkama imeona ni muhimu kuwajengea uelewa ili waweze kusaidia jamii kupata taarifa sahihi na kuwaelekeza wananchi kwenye njia zinazofaa za kutafuta haki\r\nAidha, Mhe. Khamis amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa sehemu ya mchakato wa mabadiliko ya Mahkama, akieleza kuwa wananchi ni wadau muhimu wa Mahkama kwa kuwa uwepo wao ndio msingi wa Mahkama kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa haki.\r\nVilevile, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa wanayoyapata katika kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma na maboresho yanayofanywa na Mahkama.\r\nKatika mafunzo hayo, jumla ya mada tatu ziliwasilishwa, ambazo ni Mfumo wa Usikilizaji wa Mashauri kwa Njia ya Kielektroniki, Mabadiliko ya Mahkama katika Masuala ya Jinsia, pamoja na Mfumo wa Ukaguzi na Usimamizi wa Maadili katika Mhimili wa Mahkama. Mada hizo zililenga kuwawezesha washiriki kuelewa mwelekeo wa mabadiliko yanayofanyika katika Mahkama na namna wanavyoweza kushiriki katika kuyafanikisha.\r\nMafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mahkama ya Zanzibar za kuimarisha ushirikiano na wadau katika kuboresha utoaji wa huduma za haki na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma, mifumo na mabadiliko yanayoendelea ndani ya Mahkama. Mabadiliko hayo yote yanafanyika chini ya Mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP) unaofashiliwa na Benki ya Dunia (World Bank).