RAIS MWINYI UJIO WA MAJAJI WAKUU WA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA ZANZIBAR NI ISHARA YA AMANI, UONGOZI BORA NA MSHIKAMANO
2026-10-05
Zanzibar Judiciary
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kufanyika kwa Mkutano wa Majaji Wakuu wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (SEACJF) Zanzibar ni ishara ya uwepo wa amani, uongozi bora na mshikamano, pamoja na kuimarika kwa ushirikiano baina ya nchi za Afrika.\r\nRais Mwinyi ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), unaofanyika katika Hoteli ya Verde, Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026.\r\nAmesema uwepo wa Majaji Wakuu na viongozi waandamizi wa Mahkama kutoka nchi mbalimbali za ukanda huo unatoa fursa muhimu ya kuimarisha umoja na ushirikiano, pamoja na kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuboresha mifumo ya utoaji haki.\r\nRais Mwinyi ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa nchi wanachama kujadili mageuzi ya kimahakama, kuimarisha ufanisi katika utoaji wa haki na kutafuta suluhisho la pamoja dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya haki barani Afrika.\r\nAidha, amesema majadiliano ya mkutano huo yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhalifu wa kiuchumi, ambao umeendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazozikabili nchi nyingi, hususan barani Afrika.\r\nAmesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi, hususan katika mifumo ya sheria na Mahkama, ili kuwezesha mapambano dhidi ya uhalifu wa kiuchumi na aina nyingine za uhalifu unaovuka mipaka kufanyika kwa ufanisi zaidi.\r\nVilevile, Rais Mwinyi amesisitiza umuhimu wa uhuru wa Mahkama, akieleza kuwa Mahakama huru ni nguzo muhimu katika kuhakikisha haki inatolewa kwa mujibu wa sheria, bila upendeleo wala kuingiliwa, na hivyo kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki.\r\nRais Mwinyi amehakikishia washiriki kuwa Zanzibar itaendelea kuunga mkono juhudi na mipango inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda, utawala wa sheria na maendeleo ya mifumo ya haki, kwa manufaa ya wananchi wa Afrika na dunia kwa ujumla.\r\nNaye Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amesema ushirikiano baina ya Majaji Wakuu wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika una umuhimu mkubwa katika kuimarisha uwajibikaji ndani ya taasisi za Mahakama, kuongeza ufanisi wa mifumo ya utoaji haki na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.\r\nMhe. Jaji Mkuu amesema mkutano huo unatoa fursa muhimu kwa Mahakama za nchi wanachama kujadili mageuzi yanayoendelea katika sekta ya haki, yakiwemo matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa Mahakama, usimamizi wa mashauri na uboreshaji wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.\r\nAidha, amesema Zanzibar itanufaika na uzoefu wa nchi mbalimbali kupitia majadiliano na kubadilishana maarifa, pamoja na kujifunza mbinu bora zinazotumika katika uendeshaji na usimamizi wa Mahakama.\r\nAmeeleza kuwa mikutano ya aina hiyo ni muhimu kwa kuwa inawakutanisha viongozi wa Mahakama kujadili changamoto zinazofanana katika mifumo ya utoaji haki na kutafuta kwa pamoja suluhisho na mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo.\r\nMhe. Jaji Mkuu amesisitiza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria, kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa Mahakama, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa usawa.