JAJI MKUU WA ZANZIBAR AFUNGUA KIKAO KAZI CHA KUTAFSIRI SHERIA YA MWENENDO WA MADAI KWA LUGHA YA KISWAHILI
2026-11-02
Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amefungua kikao kazi cha Kamati ya Wataalamu wa Kutafsiri kwa Lugha ya Kiswahili Rasimu ya Sheria Mpya ya Mwenendo wa Madai Zanzibar, akieleza kuwa sheria hiyo inalenga kuleta maboresho makubwa katika mfumo wa utoaji wa haki kwa kuzingatia mabadiliko ya kijamii, maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya sekta ya sheria.\r\nAkizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho uliofanyika tarehe 02 Novemba, 2026, katika Hoteli ya Visitors Inn, Jambiani, Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Jaji Mkuu amesema kuwa Sheria ya Mwenendo wa Madai inayotumika sasa ilitungwa mwaka 1917 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1974. Ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika jamii na maendeleo ya sayansi na teknolojia, sheria hiyo imepitwa na wakati na hivyo kuhitaji kufanyiwa maboresho ili kukidhi mahitaji ya sasa ya utoaji wa haki.\r\nMhe. Jaji Mkuu amefafanua kuwa rasimu ya sheria hiyo mpya imejumuisha masuala mbalimbali muhimu, yakiwemo utatuzi mbadala wa migogoro (ADR), haki za kidijitali, taratibu maalumu za uendeshaji wa mashauri pamoja na maeneo mengine yanayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi katika upatikanaji wa haki kwa wananchi.\r\nAidha, amesema kuwa kutafsiri sheria hiyo kwa lugha ya Kiswahili inaendana na matakwa ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Serikali kwa ujumla ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuelewa sheria zinazowaongoza na zinazohusu haki zao pamoja na wajibu wao mbele ya sheria.\r\nVilevile, Mhe. Jaji Mkuu amewapongeza na kuwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kujitolea muda wao na kuweka pembeni majukumu mengine ili kushiriki katika kazi hiyo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya sheria nchini Zanzibar.\r\nAmeeleza kuwa mchango wa wataalamu hao una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha tafsiri ya sheria hiyo inakuwa na ubora unaotakiwa, inazingatia usahihi wa maana za kisheria na matumizi sanifu ya lugha ya Kiswahili, bila kupotosha dhamira na madhumuni ya vifungu vya sheria husika.\r\nKikao kazi hicho kimewakutanisha wataalamu mbalimbali wa sheria pamoja na wabobezi wa lugha ya Kiswahili, akiwemo mwandishi mashuhuri Shafi Adam Shafi, Profesa Issa Haji Zidi, Profesa Moh'd Makame Haji na wataalamu wengine.