KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI YAFANYA ZIARA YA KUANGALIA MAENDELEO YA UJENZI WA MAHKAMA ZA KIJICHI, TUNGUU NA MAKUNDUCHI
2026-11-10
Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla ameiomba Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa kuendelea kuunga mkono juhudi za Mahkama ya Zanzibar katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa majengo ya Mahkama unaolenga kuboresha mazingira na huduma za utoaji haki kwa wananchi.\r\nJaji Mkuu ameyasema hayo alipotembelewa na Kamati hiyo kwa lengo la kumsalimia ofisini kwake Tunguu, Zanzibar tarehe 10 Novemba, 2026 mara baada ya ziara ya kutembelea maeneo ya Kijichi na Tunguu. \r\nAidha, Jaji Mkuu ameishukuru Kamati hiyo kwa ushirikiano na mchango wake katika kuunga mkono jitihada za Mahkama ya Zanzibar, ambazo zimechangia kufanikisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahkama katika maeneo mbalimbali. Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.\r\nJaji Mkuu pia amesisitiza dhamira ya Mahkama ya Zanzibar ya kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inasimamiwa ipasavyo ili iweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa. Ameeleza kuwa Mahkama itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mazingira rafiki ya kupata haki.\r\nKwa upande wake, Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Mhe. Machano Othman Said baada ya kutembelea miradi ya ujenzi ya Mahkama za Kijichi, Tunguu na Makunduchi amesema kamati imerizishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi hizo na imewasisitiza wakandarasi na wajenzi wa majengo hayo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa wakati , ambapo kwa mujibu wa mikataba iliyofungwa miradi ya ujenzi wa Mahkama za Makunduchi na Kijichi inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2027 na mradi wa ujenzi wa Mahkama Jumuishi Tunguu, unatarajiwa kukamilika Novemba 2027.\r\nKamati hiyo pia imemuomba Jaji Mkuu wa Zanzibar kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo muhimu ili kuhakikisha haikwami njiani na inakamilika kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa. Wajumbe wa Kamati wameeleza umuhimu wa miradi hiyo katika kuboresha miundombinu ya Mahkama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa wananchi.\r\nUjenzi wa Mahkama hizo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) chini ya Mradi wa Maboresho ya Mahkama ya Zanzibar (Zi-JUMP). Ziara hizo zinatarajiwa kuendelea kesho tarehe 11 Novemba, 2026 kwa maeneo yanayojengwa Mahkama za Kinduni, Nungwi na Ukarabati wa Mhkama ya Watoto Mahonda.